Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi Msaidizi wa Pembejeo wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Shenal Nyoni.
Majaliwa amesema kuwa sababu ya kumsimamisha mkurugenzi ni kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili kwa kuongeza gharama za pembejeo kwa kushirikiana na baadhi ya mawakala.
Waziri mkuu amesema Serikali italipa madeni yote ya mawakala wa pembejeo za kilimo mara baada ya kukamilisha uhakiki na kujiridhisha juu ya uhalali wake, sababu bado inawahitaji mawakala ili kushirikiana nao katika kuhudumia wakulima kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo katika kikao alichokiitisha kwenye Makazi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma kati yake na mawakala wa pembejeo za kilimo pamona na Maofisa kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Waziri Mkuu ameongeza mawakala wa pembejeo waliwasilisha Serikali deni la sh. bilioni 65.4 kwa huduma waliyoitoa katika mikoa 25 ambapo Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi imekamilisha uhakiki wa madeni hayo kwa mikoa 10 ya Morogoro, Iringa, Njombe, Ruvuma, Songwe, Rukwa, Katavi, Kigoma, Kilimanjaro na Arusha ambayo madeni yake ni asilimia 70 ya madeni yote.
Amesema ripoti ya uhakiki wa mikoa nane kati ya 10 imetoka (imebaki Katavi na Kigoma) na kubainisha kuwa mikoa hiyo inadai sh. bilioni 36 kati ya hizo sh. bilioni 11 bado zinaendelea kuhakikiwa, sh. bilioni 14 zimekataliwa hivyo siyo madeni halali, sh. bilioni 8.2 ndiyo deni halali na sh. bilioni 2.3 zinachungizwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).