Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), amewaonya watendaji wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), wanaonea wafanyabiashara wakati wa ukusanyaji wa mapato.
Amesema mwenendo wa makusanyo mkoani hapa hayaridhishi kwani TRA wamegeuka kuwa jeshi, wanaonea na kudhalilisha watu pindi wanapokwenda kukusanya mapato.
Lema amesema kuwa ukali na umakini wa Rais Magufuli, umesaidia katika baadhi ya mambo, lakini pia umetumika kuongeza wigo mkubwa wa rushwa kwani kuna baadhi ya watendaji wanatumia nafasi hiyo kujinufaisha, kuwaomba kwa kuwalazimisha wafanyabiashara kuchangia masuala mbalimbali katika jamii.
Amesema kuwa hali hiyo ikiendelea itasababisha ukusanyaji wa mapato nchini kushuka kwani wafanyabiashara hawatakuwa na ujasiri wa kuwekeza, mauzo yatapungua wakati kodi inapatikana kupitia mauzo.
Lema alidai kuwa baadhi ya baa jijini hapa zimekuwa zikivamiwa usiku na TRA wakiwa na polisi na kwenda kwenye droo za kaunta na kuangalia mauzo wakidai risiti na kwamba TRA wamegeuka kuwa waasi badala ya kukusanya kodi, hali inayosababisha usumbufu kwa wafanyabiashara.