Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amesema kuwa kamati ya kinga, haki na madaraka ya bunge ilimuhoji juu ya kauli nne alizotoa baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa wabunge wa Afrika Mashariki (EALA), ambao wagombea wawili wa Chadema, Lawrence Masha na Ezekia Wenje, walipigiwa kura za hapana.
Mbowe amesema kauli hizo ni pamoja na aliyosema Ndugai amevunja kanuni na sheria hazikufuatwa katika uchaguzi huo, mchakato wa uchaguzi huo ulikuwa ni mkakati wa Serikali na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alikuwa anajua, wagombea Chadema walikuwa wazuri lakini kupigwa kura ya hapana ilikuwa ni mkakati wa CCM na ya nne uchaguzi ulikuwa batili.
“Walinihoji kwamba Aprili 4, mwaka huu baada ya kufanyika uchaguzi wa EALA, nikiwa nje ya ukumbi wa Bunge nilidhalilisha mamlaka ya Spika na Bunge.
“Sasa katika maelekezo yangu niliwaambia kwamba kauli hizo nilizitoa baada ya mabishano marefu mle ndani (ndani ya ukumbi wa Bunge) na kwamba mimi ni kiongozi, lakini leo (jana) sijajua kwanini wagombea wetu walikataliwa. Je, hawana elimu au hawajui Kiingereza?
“Niliwaambia sikudharau Bunge wala kiti cha Spika, mimi ni mbunge wa muda mrefu, ninajua utaratibu wa Bunge. Nikawaambia kauli yangu haikulenga mtu binafsi bali nililalamikia uchaguzi, lakini wanadhani nilimlenga mtu binafsi, nimeomba radhi, lakini bado msimamo wangu uko palepale,.
Mbowe na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), jana wamehojiwa na Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge kwa muda wa saa mbili – saa moja kila mmoja.