Wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga jijini Dar es salaam wamekumbwa na taharuki baada ya kufika katika eneo lao la biashara nje ya jengo la Machinga complex na kukuta vibanda vyao vimebomolewa.
Zoezi hilo limefanyika usiku wa kuamkia Jumatatu na kwa hasira wafanyabiashara hao wakachoma moto barabara kwa kutumia matairi na takataka nyingine.
Wafanyabiashara hao wamedai kuwa walipewa siku tatu kuhakikisha wanaondoa bidhaa zzao hata hivyo waliandika barua ya kuomba kusitishwa kwa zoezi hilo ili wapatiwe vizimba lakini cha kushangaza ni kwamba wamevunjiwa hata bila kupata majibu ya baraua yao.
Pia wamelalamika kupotea kwa bidhaa zao ambazo baadhi yake zimeibiwa na nyingine hawajui zimepelekwa wapi.
Mfanyabiashara wa machinga Complex Yohana William amelalamika kuwa mtaji wake wote umepotea kwani alikuwa ameaminiwa na mali za watu kufanya biashara lakini vunjavunja hii imemharibia biashara yake na amepoteza kila kitu.