Rais wa Marekani, Donald Trump amedai kuwa taifa hilo litko tayari ‘kutatua’ tishio la nyuklia kutoka Korea Kaskazini kwa ushirikiano au bila ushirikiano na China.

‘Endapo China itashindwa kutatua suala la Korea Kaskazini, tutalitatua. Hicho ndicho ninachowaambia’. Rais Trump ameyasema hayo alipokuwa akifanya mahojiano na gazeti la Uingereza la Financial Times.

Alipoulizwa endapo anafikiri kuwa anaweza kufanikiwa peke yake, rais Trump alijibu ‘Hakika’.

Rais Trump alikuwa akizungumza na gazeti hilo kabla ya ziara ya rais wa China, Xi Jinping ambaye anatarajiwa kutembelea Marekani wiki hii.

Rais Trump pia alinukuliwa akilieleza shirika la habari la FT: ‘China ina ushawishi mkubwa kwa Korea Kaskazini. Na China inaweza kuamua kutusaidia au kutokutusaidia. Wakitusaidia itakuwa jambo zuri sana kwa China na wasipofanya hivyo haitokuwa na faida kwa yeyote’

Kauli hizo za rais Trump zinahofiwa huenda zikadhoofisha uhusiano wa kibiashara baina ya mataifa hayo yenye uchumi mkubwa zaidi dunia huku rais Trump akiandika ujumbe kwenye mtandao wa Twitter:

‘the meeting next week with China will be a very difficult one in that we can no longer have massive trade deficits’.

China ndio taifa pekee lenye uhusiano wa kidiplomasia na nchi ya Korea Kaskazini.

Kabla ya mkutano wa juma hili mjini Florida, washauri wa masuala ya usalama nchini Marekani wameelezwa kuharakisha kukamilisha orodha ya sera zilizopendekezwa.

Katika ziara yake ya kwanza katika bara la Asia, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Rex Tillerson amesema diplomasia ya miaka 20 ya nchi za magharibi iliyolenga kuidhibiti Korea kaskazini imeshindwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *