Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegn amemhakikishia Rais Magufuli kuwa nchi yake ipo tayari kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania utakaosaidia kuleta manufaa makubwa zaidi kiuchumi na kukabili umasikini.
Hailemariam Dessalegn ametoa kauli hiyo leo Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wananchi wa Tanzania na Ethiopia kupitia vyombo vya habari muda mfupi baada ya kuwasili nchini kwa ziara rasmi ya kiserikali ya siku mbili, anayoifanya kwa mwaliko wa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Hailemariam Dessalegn amesema atatilia mkazo ni ushirikiano katika usafiri wa anga ambapo ameahidi kuwatuma wataalamu kutoka Shirika la Ndege la Ethiopia kuja nchini kushirikiana na Wataalamu wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ili kuimarisha utendaji kazi na kuikuza ATCL.
Pia amesema Shirika la Ndege la Ethiopia kwa kushirikiana na ATCL litaufanya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam kuwa kituo chake cha mizigo (Cargo Hub) na hivyo kuwezesha mizigo ya ukanda wa Afrika Mashariki na maeneo jirani kutumia uwanja huo kusafirisha mizigo yake duniani kote.
Rais Magufuli na Hailemariam Dessalegn ambao kabla ya kuzungumza na wananchi wamefanya mazungumzo rasmi, wamesema wamekubaliana kuwa Tanzania na Ethiopia zibadilishane uzoefu juu ya uzalishaji wa nishati ya umeme kwa kutumia maji ambapo Mhe.
Hailemariam Dessalegn ameahidi kuwatuma wataalamu wa nchi yake kuja nchini Tanzania kutoa uzoefu wa namna Ethiopia ilivyoweza kuzalisha kiasi kikubwa cha umeme kwa kutumia maji ukiwemo mradi mkubwa unaoendelea kujengwa uitwao Grand Ethiopian Renaissance Dam(GERD) ambao unatarajiwa kuzalisha megawatts 6,470 za umeme.