Mshauri wa zamani wa usalama wa rais Donald Trump, Michael Flynn ameomba kupatiwa kinga ya kutoshtakiwa ili aweze kutoa ushahidi kuhusiana na tuhuma za Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani.
Kwa mujibu wa mwanasheria wa Flynn, Robert Kelner mwanajeshi huyo mstaafu ‘ana jambo la kueleza’ lakini anahitaji ulinzi dhidi ya ‘mashtaka ya uonevu’.
Bunge la Congress linaendelea kuchunguza madai hayo huku mmoja wa maseneta wa bunge hilo akionya kuwa kuhusiana na ikulu ya Urusi, Kremlin kuwa ‘Propaganda imesambaa kila sehemu’.
Flynn alifukuzwa kazi mwezi Februari baada ya kutoa taarifa za kuipotosha ikulu ya Marekani kuhusiana na mazungumzo yake na mwakilishi wa Urusi.
Uhusiano wake na Urusi umekuwa ukichunguzwa na FBI na Kamati ya Usalama ya Bunge na Baraza la Maseneta ikiwa ni sehemu ya uchunguzi kuhusu madai ya Urusi kujaribu kusaidia ushindi wa Donald Trump kwenye uchaguzi mkuu huku pia mawasiliano ya baadhi ya maofisa wa kampeni za Trump wakichunguzwa kwa mawasiliano na maafisa wa Urusi.