Aliyekuwa katibu mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dkt. Willbrod Slaa amepongeza utendaji kazi wa Serikali ya Rais Magufuli.
Mbunge huyo wa zamani wa Karatu amesema kuwa watu waelewe hakuna nchi hata moja ambapo kiongozi atakubalika na watu wote kwa asilimia 100.
Dkt. Slaa amesema wako watu ambao masilahi yao yataguswa kwa namna moja au nyingine hivyo lazima watapiga kelele.
Kutokana hilo, alisema Rais Dk. Magufuli katika kundi ambalo halihitaji fedha ameyatekeleza yote kwa asilimia 99.9, ikiwa ni pamoja na uwajibikaji serikalini, kuchukua hatua kali dhidi ya rushwa, uwizi wa mali za umma, uwindaji haramu na kudhibiti dawa za kulevya.
Slaa amesema kuwa kwa bahati mbaya mchwa wengine waliopenya mpaka ndani ya Ikulu na Serikali na huwezi kufagia Serikali nzima kwa siku mmoja.
Dkt. Slaa ambaye kwasasa anaishi nchini Canada na familia yake amesema kuwa “Kwa jinsi Rais ambavyo hayumbi na wala hayumbishwi, nina hakika atafikia malengo na kurudisha Taifa kwenye misingi ya tunu za Taifa ya uwazi, ukweli, uadilifu, kuheshimiana na kuthaminiana na hasa kujali utu.
Pia ameongeza kwa kusema kuwa “Hii ndiyo hali ambayo JPM kila siku anaiita ‘Transition’ (kipindi cha mpito). Tutafika tu, tunatakiwa kuwa wavumilivu na wenye uzalendo wa kweli ana nia njema ya kufikisha Taifa mahali pazuri. Hii inahitaji kuweka pembeni maslahi yetu binafsi kama mtu mmoja mmoja, viongozi wa Serikali au hata wa kisiasa,”.