Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nay wa Mitego jana amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe mjini Dodoma.

Waziri huyo alimtaka Nay wakutane mjini Dodoma baada ya kuamuru kuachiwa kwa mwanamuziki huyo baada ya kukamatwa na Polisi kutokana na wimbo wake ‘Wapo’ kuikashifu Serikali iliyopo Madarakani.

Katika mazungumzo hayo, Dkt Mwakyembe amesema wasanii wana nafasi kubwa katika kuisaidia serikali kukemea mambo maovu bila kuvuka mipaka.

Mwakyembe amewataka vijana nchini kutambua kuwa Tanzania ni nchi inayozingatia utawala wa sheria na kwamba wana uhuru wa kukosoa bila kutukana au kwenda nje ya maadili.

Pia waziri Dkt. Mwakyembe amesisitiza kuwa serikali haiwezi kuwanyima watu uhuru wa kujieleza ilimradi tu wasivuke mipaka.

Kwa upande wake Nay alimshukuru Rais Magufuli kwa kuwa mwelewa, kitu ambacho hakuwa ametegemea huku pia akiwatetea polisi waliomkamata kwa kueleza kuwa walikuwa wakifanya kazi yao.

Baada ya kukutana na waziri wa habari jana mkoani Dodoma, Nay leo anatarajia kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *