Aliyekuwa Mbunge wa Afrika Mashariki, Shy-Rose Bhanji amelalamika jina lake kukatwa katika kinyang’anyiro cha kutetea nafasi hiyo bila kuhojiwa juu ya tuhuma zilizopeleka jina lake kukatwa.
Bhanji pia ametumia fursa hiyo kuwapongeza wanachama waliochaguliwa kuwa wagombea wa Bunge la Afrika Mashariki kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi na kuwashukuru wabunge kwa kumpigia kura zilizomuwezesha kuwa miongoni mwa wagombea wanne wa mwanzo waliopata kura nyingi zaidi.
Bhanji amesema hayo kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii “Ingawa jina langu limekatwa na Kamati Kuu ya Chama bila ya mimi nwenyewe kuitwa na kuhojiwa ili nipewe haki ya kujibu hoja zozote dhidi yangu, nawapongeza wote waliochaguliwa kuwa wagombea wa EALA kupitia CCM. Ninawashukuru sana Wabunge kwa kunipigia kura nyingi zilizoniwezesha kuwa miongoni mwa wagombea wanne wa mwanzo walioongoza kwa kura”.
Jana Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hamphrey Polepole alitangaza majina ya wagombea 12 watakaowania nafasi 6 za ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki huku jina la Bhanji likitupwa kule.
Akiyataja majina hayo mbele ya waandishi wa habari, Polepole alesema wagombea hao 12 wanane wanatoka Tanzania ambapo wanaume wanne na wanawake wanne na wagombea wanne wanatoka Zanzibar ambapo wanawake wawili na wanaume wawili.