Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imemhoji Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa saa tatu kuhusu tuhuma za kuingilia madaraka ya mhimili huo wa dola na imesema imemaliza kazi na taarifa yake itaiwasilisha kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Makonda alifika Dodoma ikiwa ni hatua ya kuitikia mwito wa kamati hiyo uliotokana na Azimio la Bunge lililotolewa na Bunge, Februari 8, mwaka huu katika kikao cha Nane cha Mkutano wa Sita wa Bunge kwamba mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam ahojiwe na Bunge.

Katika kikao hicho, Bunge liliazimia kwamba Makonda na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti waitwe mbele ya Kamati hiyo ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge ili kujibu tuhuma zinazowakabili dhidi ya mhimili huo.

Mwenyekiti wake, George Mkuchika alisema imekutana jana baada ya kuagizwa na Spika wa Bunge kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge.

Mwenyekiti huyo alisema hatua inayofuata kama ilivyo utaratibu, Kamati yake itakabidhi taarifa yake kwa Spika kwa mujibu wa Kanuni, na Spika ndiye atakayeamua namna ya kutoa taarifa kuhusu kazi ya kamati hiyo.

Mkuchika amesema Spika aliiagiza kamati hiyo imuite Makonda mbele ya kamati kutokana na azimio hilo la Bunge lililopitishwa Februari 8, ambapo pamoja na mambo mengine mkuu huyo wa mkoa alitakiwa kufika mbele ya kamati kujibu tuhuma hizo zinazomkabili.

Pia amesema kwa mujibu wa Azimio hilo, Makonda alidaiwa kutoa kauli kupitia Televisheni ya Clouds akidai kwamba wabunge wanasinzia bungeni jambo lililoonekana kwamba ni kudharau Bunge.

Source: Habari Leo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *