Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma hatoweza kuhudhuria mazishi ya mpigania haki za watu weusi nchini humo, Ahmed Kathrada baada ya familia ya mwanaharakati huyo kumuomba asihudhurie.
Mwaka jana, mwanaharakati huyo alimtaka rais Zuma kujiuzuru wadhifa wa urais kufuatia kukumbwa na mfululizo wa kashfa za rushwa.
Badala yake, makamu wa rais Cyril Ramaphosa ndiye atakayeiwakilisha serikali kwenye mazishi hayo.
Mpigania uhuru huyo aliyefungwa sambamba na hayati Nelson Mandela wakati wa harakati za kupigania uhuru wan chi hiyo, alifariki siku ya Jumanne akiwa na umri wa miaka 87.
Ahmed Kathrada alikaa kwa zaidi ya miaka 26 gerezani kabla ya kuachiwa huru mwaka 1989 na baadae kuwa mshauri wa rais wa wakati huo aliyechaguliwa kidemokrasia, hayati Nelson Mandela.
Licha ya kuwekewa pingamizi hilo lakini rais Zuma alishatoa agizo la bendera kupepea kwa nusu mlingoti na pia ameahirisha kikao na baraza la mawaziri ili maafisa wa serikali waweze kuhudhuria mazishi hayo.
Taarifa ya serikali imedai kuwa rais Zuma amekubali kutohudhuria mazishi hayo ili kutimiza matakwa ya familia hiyo.
Mke wa marehemu Katharada, Barbara Hogan, anafahamika kwa kuwa mkosoaji mkubwa wa rais Zuma.