Leo ni kumbukumbu ya kifo cha aliyekuwa gwiji wa muziki nchini Tanzania, Marehemu TX Moshi William.
Marehemu TX Moshi William alifariki Tarehe 29 Machi 2006 siku ya Jumatano majira ya saa 3 asubuhi na kuzikwa siku hiyo hiyo katika makaburi ya Keko Machungwa jijini Dar es Salaam.
Mwanamuziki huyo alizaliwa mwaka 1958 wilaya ya Korogwe mkoani Tanga na alijiunga na bendi ya Msondo Ngoma 1982 akitokea Polisi Jazz.
Wakati yupo Msondo Ngoma alitunga nyimbo kama vile Ajuza, Asha Mwanaseif, Ashibaye, Kilio cha mtu mzima, Piga Ua Talaka Utatoa, Ndoa ya Isihaka Kibene, Kaza Moyo pamoja Ajali ambayo ilikuwa ya mwisho kabla hajaaga dunia.
TX Moshi alianzisha mitindo mbalimbali katika bendi kama vile ‘Mambo Hadharani’ wakati akiwa Msondo Ngoma.
Wakati wa uhai wake mwanamuziki huyo alipitia bendi mbalimbali hapa nchini kama vile Safari Trippers, Juwata Jazz, Uda Jazz na Polisi Jazz kabla ajajiunga Msongo Ngoma.
Pia Mwanamuziki huyo enzi za uhai wake aliwahi kupata tuzo mbali mbali kama vile tuzo za Kilimanjaro Music Awards.
TX Moshi William jina lake kamili ni Shabani Mhoja Kishiwa alipewa jina la TX na aliyekuwa mtangazaji wa Radio Tanzania marehem Julius Nyaisanga kutokana na umahiri wake katika uimbaji na kutunga.
TX Moshi wakati anafariki alimuacha mke Asha Mwanaseif ambaye nae ni marehemu kwasasa pamoja na mtoto wake wa kiume Hassan Moshi maarufu kama TX Jr ambaye anaimbia bendi ya Msondo.
Tasnia ya muziki wa Dansi nchini Tanzania itamkumbuka TX Moshi kutokana na mchango wake katika muziki huo.
Pumzika kwa amani TX Moshi William.