Wizara ya Fedha na Mipango imetoa mapendekezo ya sura ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ikionesha itakusanya na kutumia Sh trilioni 31.7 ikilinganishwa na Sh trilioni 29.5 ya mwaka 2016/2017.

Katika mapendekezo hayo yaliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango, fedha zilizotengwa kwa maendeleo zimeongezeka kutoka Sh trilioni 11.820 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ikiwa ni asilimia 40 ya bajeti ya kipindi hicho hadi Sh trilioni 11.999 kwa 2017/2018 sawa na asilimia 38 ya bajeti yote.

Dk Mpango aliwasilisha mapendekezo hayo ya kiwango na ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka huo kwa wabunge kwenye Ukumbi wa Bunge mjini hapa.

Alisema katika mwaka wa fedha 2017/2018, jumla ya Sh trilioni 31.699 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika.

Mapato ya ndani ikijumuisha na mapato ya halmashauri yanatarajiwa kuwa Sh trilioni 19.97 sawa na asilimia 63 ya bajeti yote ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.5 ya kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2017.

Katika mwaka huu wa fedha wa 2016/2017, mapato ya ndani yanayojumuisha ya halmashauri yalikuwa Sh trilioni 18.46 sawa na asilimia 62.5.

Kwa mujibu wa Dk Mpango, ili kuhakikisha mapato hayo yanapatikana, serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa mapato na kuziba mianya ya uvujaji wa mapato.

Washirika wa Maendeleo

Dk Mpango alibainisha kuwa washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh trilioni 3.97 ambayo ni asilimia 12.6 ya bajeti yote.

Alisema misaada na mikopo hiyo inajumuisha fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo; mifuko ya pamoja ya kisekta; na ya kibajeti (GBS).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *