Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Baraka The Prince amesema kuwa wakati wake ukifika naye atajiingiza katika mambo ya filamu kama alivyofanya muigizaji, Hemed.
Baraka The Prince ameelezea hisia zake kwa kile anachokiamini kwa kusema yupo katika harakati za kujenga brand yake ya muziki ili itambulike vizuri katika soko huku akidai alishawahi kufuatwa na director mkongwe katika tasnia ya filamu maarufu kwa jina la Mtitu.
Mwanamuziki huyo amesema endapo siku watanzania watasikia msanii huyo ameingia rasmi huko basi wajue itakuwa moto wa kuotea mbali kwa kuwa hata video zake za muziki anazozitengeneza huwa anaigiza sana.
Kwa upande mwingine Baraka amesema hakuna ukweli wowote unaohusiana baina ya maisha yake na mashairi anayoyatumia katika wimbo zake huku akisisitiza kuwa anaimba kutokana na vitu vinavyotokea kwenye jamii inayomzunguka.
Mwanamuziki huyo kwasasa anamiliki lebo ya muziki inayokwenda kwa jina BANA ambapo anammiliki mwanamuziki, Lord Eyez kutoka Nako 2 Nako.