Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muumgano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amefanya ziara mgodi wa dhahabu wa Buzwagi uliopo Kahama mkoani Shinyanga na kuchukua sampuli za mchanga kwa lengo la kwenda kuyapima kwa wataalamu wa madini ili kubaini kiasi cha dhahabu kilichomo..
Majaliwa amesema wanataka kuona mchanga unaosafirishwa na mwekezaji huyo una kiasi gani cha dhahabu, pia Serikali inataka kufahamu kama kodi inayolipwa ni sahihi.
Waziri Mkuu amesema sera ya uwekezaji inasema mtambo huo unatakiwa uwepo nchini ili kila hatua ya uchenjuaji ifanyike hapa hapa, hivyo tunataka kujiridhisha na mwenendo wa mwekezaji na mapato tunayoyapata kama yanastahili.
Kwa upande wake Meneja Uendelezaji wa mgodi huo Bw. George Mkanza alisema mgodi huo ulionzishwa mwaka 2009 umeajiri watumishi 720 pamoja na vibarua 500.
Amesema kwa siku wanachenjua makontena matatu hadi sita ambapo katika kila kontena moja wanapata kilo tatu za madini ya dhahabu na tani nne za madini ya shaba.
Mkanza amesema wanazalisha asilimia 50 ya madini ya dhahabu na asilimia 50 ya dhahabu iko kwenye mchanga na inakuwa imechanganyika na madini ya shaba ambayo ndiyo unaosafirishwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kutenganishwa.