Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amesema kuwa mtu aliyemtishia bastola aliyekuwa waziri wa Habari, Sanaa, Utamduni na Michezo, Nape Nnauye si askari wa Jeshi la Polisi.
Nchemba amesema kuwa licha ya kutokuwa askari Polisi lakini mtu huyo amepatikana na atashughulikiwa kwa mujibu wa utaratibu wa Ulinzi na Usalama.
Waziri huyo amesema hayo jana baada ya kufungua mkutano wa kazi wa Maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi, Makamanda wa Mikoa na Wakuu wa vikosi vya Polisi unaofanyika mkoani Dodoma.
Nchemba alikataa kuelezea kwa undani kuhusu mtu huyo kwa kubainisha anatoka taasisi gani wala jina la mtuhumiwa kwa madai ya kuhofia usalama wake.
Baadhi ya taasisi za Ulinzi na Usalama nchini ni Jeshi la Wananchi la Tanzania, Usalama wa Taifa na Takukuru.
Mtu huyo alifanya tukio hilo wakati Nape anaelekea hoteli ya Protea alikopanga kukutana na waandishi wa habari baada ya kuondolewa kwenye nafasi ya uwaziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo.
Baada ya tukio hilo Waziri Nchemba alimuagiza IGP, Ernest Mangu kumtafuta mtu huyo aliyehusika kumuoneshea bastola Nape.