Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli jana amepokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Ripoti hiyo imewasilishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa Juma Assad katika hafla iliyohudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.

Ripoti hiyo imegusa maeneo mbalimbali yakiwemo ukaguzi wa hali ya hesabu za Serikali, misamaha ya kodi, ukusanyaji wa kodi na maduhuli ya Serikali, uandaaji na utekelezaji wa bajeti, hali ya deni la Taifa, usimamizi wa rasilimali watu, usimamizi wa mali na madeni ya Serikali na usimamizi na uendeshaji wa taasisi za umma zikiwemo taasisi muhimu za kifedha na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Prof. Mussa Juma Assad amesema pamoja na hatua kubwa iliyopigwa na Serikali katika kuzingatia taratibu za fedha bado kuna mapungufu mbalimbali ambayo yameendelea kujitokeza na ameshauri hatua zichukuliwe kukabiliana nayo ikiwemo kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za umma katika madini, kuiepusha TANESCO kununua umeme wa gharama kubwa, matumizi mabaya ya misamaha ya kodi na kuongeza mashine za kutoa risiti (EFD).

Akizungumza baada ya kupokea ripoti hiyo, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Ofisi ya CAG kwa kazi nzuri inayofanya na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na ofisi hiyo ili kukabiliana na mianya yote inayosababisha upotevu wa fedha za umma.

Hata Rais Magufuli amemuagiza CAG kufanya ukaguzi wa kina katika sekta ya madini na kubaini mianya yote ambayo inasababisha nchi kukosa mapato makubwa hususani katika misamaha ya kodi, mikataba mbalimbali na ulipaji wa kodi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *