Serikali mkoani Mbeya imeagiza kurejeshwa kwa wananchi eneo la mfanyabiashara maarufu mkoani humo, Simon Gatuna lililopo katika Kata ya Uyole jijini Mbeya kutokana na mfanyabiashara huyo kutokidhi vigezo vya kuendelea kumiliki eneo hilo.
Kwa mujibu wa wakazi wa Uyole, Gatuna aliwafikia mwaka 2003 na kuwaomba wampe eneo kwa ajili ya kujenga shule na kuwaahidi kuwa kila mwaka atakuwa akisomesha watoto watano wa wananchi watakaokubali kumpa eneo ili ajenge shule hiyo.
Wakazi hao walisema kutokana na hali ngumu ya kimaisha iliyowasababishia kushindwa kumudu gharama za kusomesha watoto wao, wananchi 36 walikubali kutoa maeneo yao na kumkabidhi mfanyabiashara huyo kwa makubaliano ya kusomesha watoto wao.
Hata hivyo, tofauti na makubaliano ya pande hizo mbili, Gatuna iliingia mitini na mpaka leo hajajenga shule badala yaake ameliacha eneo hilo mikononi mwa mwanamke anayetajwa kuwa dada yake ambaye amekuwa akilikodisha kwa watu mbalimbali kwa ajili ya kilimo.
Aidha, mfanyabiashara huyo pia ameonekana kuwa mjanja zaidi kwa kuwazunguka wananchi waliompa eneo kwa kuanza kushughulikia hatimiliki ili apate uhalali wa kumiliki eneo hilo kisheria.
Baadhi ya wananchi waliotoa eneo hilo walimwambia Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla kwenye mkutano wa hadhara kuwa baada ya kuona mfanyabiashara huyo haeleweki, baadhi walianza kurejea kwenye maeneo yao ili kufanya shughuli zao, ndipo alipoibuka na kuanza kuwafanyia unyama wa kuwabambikiza kesi.
Makalla, baada ya kuwasikiliza wananchi hao na kuomba majibu ya Ofisa Ardhi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Jacob Ngowi, alionesha kutoridhishwa na kuagiza mkataba baina ya pande hizo kuvunjwa rasmi na maeneo yarejeshwe kwa wananchi 36 waliojitolea awali.