Mweyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema kuwa Rais Dk. John Magufuli atakuwa kiongozi wa kwanza nchini kuvunja rekodi ya kutawala kwa kipindi cha miaka mitano badala ya 10 kama walivyofanya watangulizi wake.
Mbowe ameyasema hayo jana wakati akizindua tawi la wakereketwa wa chama hicho lililopo eneo la Mpakani, Kata ya Kwakifua, Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.
Katika hoja hiyo, Mbowe amesema Rais Magufuli ataongoza kwa muhula mmoja kwa kuwa utawala wake hauthamini utu wa binadamu, na ikiwa vinginevyo, yuko tayari kuachana na siasa.
Amesema tofauti na utawala huu, watangulizi wa kiongozi huyo walikuwa wakifanya kazi kwa waledi na kutenda haki huku wakisikiliza changamoto zilizowakabili wananchi.
Alisema kutokana na hali hiyo, chuki na manung’uniko miongoni mwa Watanzania ambao watafanya uamuzi katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020, vimeongezeka.
“Ndugu zangu hakuna kipindi cha kujenga mageuzi kama hiki, kwa sababu utawala huu umejenga simanzi na manung’uniko kwa Watanzania wengi, ambao leo hii wanapata shida kwa hali halisi ya ugumu wa maisha na kuacha kuthamini utu wa watu.
Pia amesema hivi sasa gharama za maisha kwa wananchi zimeongezeka na kipato kikipungua, huku Serikali ikiwa haina mpango wa kunusuru.
Source: Mtanzania