Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewataka wamiliki binafsi wa silaha wahakikishe wanapata mafunzo kuhusu namna ya kutumia, kutunza, kujihami, upigaji wa shabaha, kuwa na usiri wa umiliki wa silaha hiyo na kutotambulika na mtu mwingine.
Kamanda wa Kanda hiyo, Simon Sirro amesema jeshi hilo limefikia hatua hiyo baada ya kuwepo kwa taarifa nyingi za uporwaji wa silaha hizo zinazomilikiwa na watu binafsi ambazo hatimaye hutumika katika matukio mbalimbali ya kihalifu hapa jijini.
Simon Sirro amesema kuwa “Wamiliki wanatakiwa kuwa na utamaduni wa kuhudhuria mafunzo ya upigaji shabaha ambao utawasaidia kuwa na umakini katika kuzitumia, huna sababu ya kukaa na silaha ambayo huwezi kuitumia,”.
Katika tukio lingine, jeshi hilo limemkamata mtuhumiwa mmoja aliyefahamika kwa jina la Joseph Katundu (24) akiwa na bastola moja aina ya Luger yenye namba 07A 367486, namba za usajili TZ CAR 88626 ikiwa na risasi moja kwenye chemba.
Amesema tukio hilo lilitokea Machi 18, mwaka huu huko maeneo ya Tandale Sokoni kwenye baa inayojulikana kama Tandale Inn.