Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amedaiwa kuwatishia kuwafunga jela miezi 6 au kuwapa tuhuma za dawa za kulevya bila kupitia mahakamani wafanyakazi wa kituo cha utangazaji cha Clouds kwa kukataa kurusha habari aliyoitaka.

Hayo yamebainika katika ripoti ya uchunguzi wa tukio la mkuu huyo wa mkoa kuvamia katika kituo cha utangazaji cha Clouds akiwa na askari wenye silaha, ripoti ambayo pia imependekeza mamlaka husika kumchukulia hatua za kinidhamu.

Mwakilishi wa Kamati ya uchunguzi Deodatusi Balile amesema kamati hiyo haikuweza kumpata Paul Makonda kwa ajili ya mahojiano.

Pia amesema kamati imebaini kuingiliwa kwa uhuru wa habari kinyume cha sheria kwa kulazimisha kutangazwa kwa habari isiyokidhi vigezo.

Kuhusu wafanyakazi kupigwa, Balile amesema kamati hiyo haikuona uthibitisho wowote kuwa kuna watu walipigwa, isipokuwa wapo waliolia kutokana na vitisho vya kupelekwa jela miezi 6.

Kamati hiyo imetoa mapendekezo manne ikiwa ni pamoja kumtaka Makonda aombe radhi kwa tasnia ya habari, kumtaka Waziri kuwasilisha malalamiko kwa mamlaka yake ya uteuzi ili hatua zichukuliwe, vyombo vya dola vianzishe uchunguzi wa ndani dhidi ya askari walioingia.

Amesema kamati hiyo imejiridhisha kuwa Makonda hakuwa tayari kuhojiwa wala kutumia fursa ya kujieleza jambo ambalo hata hivyo halikuathiri uchunguzi wa kamati hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *