Timu iliyoundwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ya kuchunguza suala la kilichotokea Clouds Media Group wiki iliyopita, haijakamilisha kazi yake hadi kufikia jana usiku.

Waziri Nape aliunda timu hiyo ya watu watano juzi ikiongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dk Hassan Abbas, na aliipa muda wa saa 24 hadi iwe imekamilisha kazi yake.

Hata hivyo hadi muda uliotarajiwa na wengi wa kutoka ripoti hiyo ulipokuwa unapita timu hiyo ilikuwa haijawasilisha taarifa yake kwa waziri huyo na hakukuwa na taarifa rasmi kuhusu kushindwa kutolewa kwa taarifa hiyo.

Waziri Nape aliandika kwenye akaunti yake ya mtandao wa Twitter: ‘Kuna simu nyingi juu ya ripoti. Nawaomba tutulie Kamati wanamaliza kazi yao, ikikamilika tutaarifiwa muda na mahali nitakapokabidhiwa.’

Juzi baada ya kutembelea ofisi za Clouds Media Group, waziri Nape alisikitishwa na kitendo kilichotokea na kuahidi kufanyia kazi haraka iwezekanavyo.

Waziri Nape aliunda timu ya watu watano iliyoongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Dk Abbas Hassan, Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mabel Masasi, Mhariri Mwandamizi kutoka Kampuni ya The Guardian, Jesse Kwayu, Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Jamhuri na Mhariri wa Wapo Radio na Neng’ida Johannes.

Waziri Nape amesema ingawa serikali imesikitishwa na jambo hilo, lakini ni lazima kutenda haki kwa kumsikiliza pia mkuu wa mkoa na watu wake ili kujiridhisha halafu ndipo hatua nyingine zitakapoweza kuchukuliwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *