Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kupitia akaunti yake ya Twitter ameandika kuwa leo atakwenda katika Ofisi za Clouds Media Group kujua kilichotokea baada ya kuwapo taarifa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuwa ofisi hizo zilivamiwa.
Taarifa hizo zinadai kuwa ofisi za Clouds Media Group zilizopo Mikocheni B Dar es Salaam, zilivamiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda Usiku wa Machi 17 mwaka huu.
Taarifa hizo zinadai kuwa, RC Makonda alikuwa ameambatana na Askari wakiwa na silaha ambapo aliwashinikiza watangazaji wa kipindi cha De Weekend Chat Show kurusha mkanda wa video aliorekodiwa mwanamke mmoja na anayedai kuwa alizaa na Askofu Gwajima.
Waziri Nape amesema kuwa yeye kama kiongozi mwenye dhamana na tasnia ya habari, atakwenda ili afahamu ukweli wa mambo kuhusu hasa kilichotokea.
Waziri Nape ameandika kama ifuatavyo “Kesho asubuhi kama Waziri Mwenye dhamana na HABARI nitatembelea CloudsMedia kujua kilichotokea.Nawaomba sana wanahabari nchini KUTULIA kwasasa”.