Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Dk Jesca Msambatavangu amekiri kumuunga mkono, Edward Lowassa ndani ya CCM kabla ajahama chama.
Dk. Jesca amesema kuwa walimuunga mkono Lowassa wakijua hiyo haikuwa dhambi kwa kuwa ni mwanaCCM mwenzao wakati huo na waliamini angeweza kupokea kijiti kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete na kusukuma gurudumu la maendeleo ya Taifa mbele zaidi.
Amesema kama ambavyo wao waliamua kumuunga mkono Lowassa wapo wana CCM wengine waliwaunga mkono wagombea wengine kwa mujibu wa taratibu za chama hicho na ndio sababu wengi walijitokeza kugombea nafasi hiyo.
Pia amesema baada ya CCM kukamilisha mchakato wa kumpata mgombea wao walikuwepo waliohama chama hicho lakini yeye na wanaCCM wengine wengi waliokuwa wanamuunga mkono Lowassa walibaki na kukisaidia chama kupata ushindi kwa sababu huo ndio wajibu wao.
Kuhusu suala la kufukuzwa uanachama, Dk. Msambatavanga amesema kuwa maamuzi ya kufukuzwa uanachama yaliyofanywa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, hakuyapokea kwa mshtuko mkubwa kwa sababu alisikia taarifa hizo zikisemwasemwa kabla ya kikao hicho.
Pamoja na kwamba hajui tuhuma iliyomfukuzisha uanachama kwa kuwa hajapewa rasmi barua ya kufukuzwa amesema taratibu zilizofikia maamuzi hayo zilifuatwa.