Mjane wa aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, marehemu Nelson Mandela, Graca Machel, amekemea ndoa za utotoni na ukeketaji kwa watoto wa kike, unaoendelezwa na baadhi ya mila za makabila hapa nchini.
Kauli hiyo aliitoa wilayani Butihama mkoani Mara alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Nyamisisi.
Alisema suala la ukeketaji halitakiwi kupewa nafasi kwani linaminya haki za mtoto wa kike kwa hiyo vitendo hivyo kwasasa havifai.
Graca Machel ambaye pia ni mjane wa aliyekuwa Rais wa Msumbiji, Samora Machel yupo mkoani Mara kwa ziara ya siku tatu, kutembelea mradi wa watoto walio nje ya mfumo wa shule unaotekelezwa na Mara Alliance na Graca Machel Trust Fund.
Amesema lengo la ziara yake ni kujionea watoto walioibuliwa na mradi huo, hususan walioko chini ya umri wa miaka saba hadi 17, kuzungumza nao na kuangalia changamoto zinazowakabili.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Anna Nyamubi, amesema kuna mahitaji ya vyumba 1,762 vya madarasa, huku idadi ya wanafunzi ikiwa 6,480.