Timu ya taifa ya Malawi imetangaza kujiondoa katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2019 kutokana na ukata wa kifedha.
Taifa hilo limechukua hatua hiyo kutokana na matatizo ya kifedha pamoja na kukosa mkufunzi wa timu ya taifa.
Shirikisho la Soka la Malawi lilitoa taarifa baada ya kunyimwa idhini ya kumwajiri kocha kutoka nje na serikali ya nchi hiyo.
Shirikisho hilo lilitaka kumwajiri kocha kutoka nje ya nchi ambaye angelipwa mshahara kwa ubia wa nusu nusu kati ya shirikisho hilo na serikali.
Baada ya mashauriano ya miezi kadha, serikali kupitia Wizara ya Michezo ilikataa pendekezo la shirikisho hilo kwa misingi ya kifedha.
Kamati kuu tendaji ya shirikisho hilo ndipo ikafikia uamuzi wa kuondoa taifa hilo kutoka kwa michuano hiyo.
Malawi walipangiwa kucheza nyumbani na mshindi wa mechi kati ya Comoros na Mauritius 13 Juni mechi yao ya kwanza ya kufuzu kwa AFCON 2019.