Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete leo anatarajiwa kuzindua Taasisi ya Maendeleo ya Jakaya Mrisho Kikwete (JMKF).
Uzinduzi huo utafanyika leo jijini Dar es Salaam na baada ya uzinduzi huo, Kikwete ataendesha kikao cha kwanza cha bodi ya taasisi hiyo.
Taasisi hiyo imeundwa ili kusaidia Tanzania na Afrika katika kuimarisha amani, afya, utawala bora na maendeleo endelevu.
Aidha taasisi hiyo itajikita katika maendeleo endelevu kwa kusaidiana na wadau wengine kukabiliana na umaskini, kusaidia mkulima mdogo, kulinda mazingira na kukabiliana na athari za tabianchi.
Taasisi hiyo itasaidia pia katika afya ya mama na mtoto, kukabiliana na ugonjwa wa malaria na kuboresha lishe ya wananchi.Katika elimu, itaboresha elimu katika kuwasaidia wajasiriamali kwa mafunzo na pia itasaidia katika utawala bora na utafutaji amani.
Taasisi hiyo imesajiliwa na itakuwa chini ya uongozi wa bodi ya wadhamini wa kimataifa yenye wajumbe kutoka ndani na nje ya Tanzania ikiwemo Guinea Bissau na Marekani.
Wajumbe kutoka Tanzania ni aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala, Daktari Bingwa wa Upasuaji Profesa William Mahalu, Balozi Mwanaidi Maajar, Genevive Sangundi na Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Makampuni ya SS Bakhresa, Abubakar Bakhresa.