Vinasaba vya faru John vinatarajiwa kupelekwa nchini Afrika Kusini kwa vipimo vya vinasaba (DNA ) muda wowote kuanzia wiki hii baada kupatikana kwa mfadhili wa kulipia gharama za vipimo hivyo,
Faru John alizua gumzo nchini mwishoni mwa mwaka jana baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kufanya ziara katika Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro (NCAA) na kuwatuhumu maofisa wa shirika hilo na wale wa Idara ya Wanyamapori kwa ‘kumuuza’ faru John kwa kampuni ya Grumeti kwa takriban shilingi milioni 200.
Kutokana na tuhuma hizo maofisa zaidi ya watano kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Idara ya Wanyapori na Tawiri walitiwa mbaroni kwa mahojiano na vyombo vya usalama. Hata hivyo, baada ya muda maofisa hao waliachiwa huru.
Kampuni hiyo ya Grumeti ambayo imewekeza katika shughuli za biashara ya hoteli, utalii na uhifadhi inamiliki hifadhi ndogo (sanctuary) ya Faru Weusi pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Aidha katika mfululizo wa matukio kuhusu sakata la faru huyo baadaye ilibainika alifariki dunia Agosti mwaka jana na waziri mkuu aliunda kamati maalumu kuchunguza kifo chake na pia kupimwa DNA.
Taarifa zilizofika kutoka ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii zimeeleza kuwa tayari nyaraka zote muhimu kuhusu kupelekwa kwa vipimo hivyo nchini humo zimekamilika.