Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, ameilaumu Ujerumani kwa kuunga mkono vitendo vya ugaidi nchini kwake.
Uturuki imemfungulia mashtaka mwandishi wa habari wa Ujerumani, Deniz Yucel yanayohusiana na kuendeleza propaganda kukiunga mkono chama cha kigaidi.
Mwandishi huyo anashtakiwa pia kwa kuunga mkono vuguvugu linaloendelezwa na kiongozi wa kidini Sheikh Fethullah Gulen aliye uhamishoni nchini Marekani.
Gulen anatuhumiwa na rais Erdogan kuhusika na jaribio la mapinduzi la mwezi Julai mwaka jana lililoshindikana.
Rais Erdogan na wizara ya mambo ya nje ya Uturuki wamekasirishwa na maamuzi yaliyopitishwa ya kufuta mikutano katika miji kadhaa nchini Ujerumani iliyopangwa kuhutubiwa na mawaziri wa Uturuki.
Mikutano hiyo ilikuwa ni sehemu ya kuwashawishi raia wa Uturuki wapatao milioni 1.5 wenye haki ya kupiga kura miongoni mwa Waturuki milioni 3 wanaoishi nchini Ujerumani.