Mkali wa ‘Marry You’ Diamond Platnum amesema kuwa wimbo wa ‘Salome’ hauna matusi bali umebeba lugha ya mahaba kwenye mashairi yake.
Diamond amefunguka hayo baada ya baaadhi ya mashabiki kudai kuwa mwanamuziki huyo ametumia lugha ya matusi kwenye mistari ya wimbo huo aliomshirikisha Ray Vanny.
Diamond amesema kuwa unapokuwa unaelezea masuala ya kimahaba utaonekana kama unatukana lakini wao wamejitahidi kadri ya uwezo wao kuelezea mahaba katika lugha ambayo ni ngumu sana mtu kuielewa.
Kwa upande wake Ray Vanny amesema kuwa pamoja na yote yanayosikika kwenye wimbo ule, wamejitahidi kutumia tafsida kuyaficha na ndio sababu wimbo ule unapendwa na watu wa rika zote na unaweza kusikilizwa hata katika jumuiya ya watu wanaoheshimiana.
Salome ni wimbo uliochukua mahadhi ya wimbo wa zamani wa Saida Kalori ‘Chambua Kama Karanga’ na umepata nafasi na mafanikio makubwa katika vituo vya runinga vya kimataifa na kuweka rekodi ya aina yake kwenye mtando wa YouTube.