Serikali imesema huduma za afya za kitaalamu zitaanza kutolewa katika hospitali ya kisasa ya Benjamin Mkapa, iliyopo Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), hivyo kuwaondoa hofu wanaohamia mkoani humu kwa sababu watapata ya uhakika.
Miongoni wa huduma zitakazopatikana kwenye hospitali hiyo ni pamoja na kipimo cha magonjwa mbalimbali ya mifumo ya fahamu, mashine ya kuchukua picha za anatomia ya mwili na kumsaidia daktari kutambua maradhi yanayomkabili mgonjwa (MRI), upasuaji kwa njia ya matundu na wataalamu bingwa wa magonjwa ya wanawake na watoto.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati alipotembelea hospitali hiyo jana ambapo pia alibainisha kuwa tayari wizara hiyo imehamia rasmi Dodoma pamoja na watumishi 106.
Pamoja na mambo mengine, alikagua mashine za kisasa zinazoendelea kufungwa katika hospitali hiyo. Ummy alisema serikali inawathibitishia Watanzania kuwa huduma zote na mahitaji ya kibingwa zitapatikana Dodoma na huduma za vipimo, hivyo itaanza Aprili mosi mwaka huu baada za mashine zote kufungwa.
Amesema hataki kuona hospitali hiyo inafanya upasuaji kwa njia ya kawaida, bali iwekeze kwenye iwekezaji wa upasuaji kwa njia ya matundu madogo.
Alisema hospitali hiyo itakuwa na kipimo cha afya ya matiti ambacho hata hospitali ya Muhimbili hakipo. Pia alisema hospitali hiyo kwa siku za usoni itaanza kutoa huduma ya kusafisha figo na wataanza na vitanda 20.