Dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema (Chadema), itajulikana Ijumaa wiki hii baada ya shauri hilo kurudishwa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kwa utekelezaji wa uamuzi wa Mahakama ya Rufaa.

Hatua hiyo imekuja baafa ya jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa Tanzania kufuta rufaa mbili za Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), dhidi ya  mbunge huyo juzi mjini hapa.

Mmoja wa mawakili anaomtetea mbunge huyo, Adam Jabir, alisema shauri hilo litaamuliwa Machi 3, mwaka huu mbele ya Jaji Salma Maghimbi kutokana na rufaa ya Jamhuri namba 135 ya mwaka jana, inayopinga uamuzi wa Novemba 11, mwaka jana wa Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Desderi Kamugisha kumpa Lema haki ya dhamana.

Novemba 11 mwaka jana, Wakili Mwandamizi wa Serikali Paul Kadushi, alisimama wakati hakimu huyo akijiandaa kuandika masharti ya dhamana na kuieleza mahakama hiyo kuwa wameshasajili notisi ya kusudio la kukata rufaa Mahakama Kuu wakipinga uamuzi wa hakimu huyo kumpa Lema dhamana.

Hata hivyo,uamuzi huo wa dhamana haukuweza kutekelezwa kwa sababu ya nia ya kukata rufaa waliyoitoa mawakili hao wa Serikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *