Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepiga kura juu ya rasimu ya azimio linalolenga kuiwekea vikwazo Syria kutokana na hatua yake ya matumizi ya silaha za sumu.
Rasimu ya azimio hilo iliyoandaliwa na Marekani, Uingereza na Ufaransa inakusudia kuwawekea vikwazo raia 11 wa Syria pamoja na taasisi 10 zinazohusishwa na mashambulizi hayo yaliyofanyika kwa kutumia silaha za sumu katika mgogoro uliochukua karibu miaka sita sasa.
Hatua hiyo pia inalenga kuzuia mauzo ya vifaa vya kijeshi pamoja na ndege za kivita kwa jeshi la Syria au serikali ya nchi hiyo.
Pendekezo hilo linafuatia uchunguzi uliofanywa na Umoja wa Mataifa uliomalizika Oktoba mwaka jana ulioihusisha Syria na matumzi ya mabomu ya mapipa kwa kutumia ndege zake za kivita kuyalenga maeneo matatu yaliyokuwa yakishikiliwa na makundi ya upinzani katika kipindi cha mwaka 2014 na 2015.
Uchunguzi huo uliofanywa na Umoja wa Mataifa ukishirikisha shirika linalohusika na kuzuia matumizi ya silaha za sumu (OPCW) pia ulibaini kundi la itikadi kali linalojiita Dola la Kiisilamu lilitumia silaha za sumu katika mashambulizi yake mnamo mwaka 2015.
Balozi mdogo wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vladimir Safronkov amesema iliyopita kuwa Urusi itatumia kura yake ya turufu kupinga hatua hiyo kwa sababu imeegemea upande mmoja na hakuna ushahidi wa kutosha.