Waigizaji wa Bongo Movie wamekanusha taarifa iliyotolewa na Wema Sepetu kuhusu kutolipwa kwa wasanii walioshiriki kwenye kampeni za CCM kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Wiki iliyopita Wema Sepetu mbele ya waandishi wa habari alisema kuwa wasanii walionda kampeni ya ya Mama Ongea na Mwanao ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hawajawalipwa pesa za kampeni walizofanya kwenye uchaguzi huo.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Protea, wasanii hao wakiongozwa na Yobnesh Yusuph ‘Batuli’ na Ndumbangwe Misayo ‘Thea’, wamesema madai aliyoyatoa Wema Sepetu hayana ukweli wowote kwa sababu wasanii wote walilipwa na Wema alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakiwalipa wasanii hao.
Mara baada ya Thea na Yobnesh kuzungumza maneno machache, mkutano huo na waandishi wa habari ulimalizika, ukiwa umechukua dakika chache tu na kuacha kila mtu akaizungumza lake.
Wema Sepetu aliibuka mbele ya wanahabari wakati akihamia Chadema kwa madai ya kufanyiwa hila kwenye CCM huku akidai kuwa Kundi la Mama Ongea na Mwanao linakidai CCM pesa yao ya kampeni waliyofanya mwaka 2015.