Jeshi ya Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewataka madereva bodaboda katika Jijini la Dar es salaam, kuacha kufanya shughuli hiyo ifikapo majira ya saa 6 usiku ili kupunguza uhalifu.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, amesema kuwa jeshi hilo limebaini wahalifu wengi hutumia mwanya katika muda huo kutenda uhalifu ikiwa ni pamoja na kuwadhuru waendesha pikipiki.
Sirro amesema, kuanzia Februari 18 hadi 23 Jeshi la Polisi Usalama Barabarani limefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 460 kutokana na makosa mbalimbali ya barabarani pamoja na kukamata pikipiki 1,280 kati ya hizo pikipiki 30 zimekamatwa kutokana na kupita katika njia ya mabasi yaendayo haraka huku madereva 27 wakifikishwa mahakamani.
Kuhusu suala la dawa za kulevya, Sirro amewaambia waandishi wa habari kuwa mpaka sasa limefanikiwa kukamata jumla watuhumiwa 257 pamoja na kete za dawa za kulevya 1,526, puli 112 na misokoto ya bangi 247 kutokana na oparesheni inayoendelea.
Amesema baadhi ya watuhumiwa bado awajafikishwa mahakamani kwani upelelezi bado haujakamilika na mara baada ya upelelezi kukamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.