Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi ameiagiza Ofisi ya Biashara ya Manispaa hiyo kushirikiana na Polisi kufanya operesheni katika vibanda vya michezo ya kubashiri “betting” na kuwakamata wanaowaruhusu watoto kushiriki michezo hiyo.

Mbali na kuwakamata wamiliki hao, pia amemuagiza Ofisa Biashara wa Manispaa hiyo, Mohamed Basama kuwasiliana na watoa leseni za mchezo huo Bodi ya Michezo ya Kubahatisha kuhakikisha wanafuta leseni za wote watakaobainika kuwaruhusu watoto kucheza mchezo huo.

Agizo hilo limekuja baada ya mkuu huyo wa wilaya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa watoto wao wamekuwa wakishindwa kusoma na wengine kujihusisha na wizi ili wapate fedha za kubeti.

Amesema baadhi ya watoto wamekuwa wakishinda katika vibanda vya kubeti kuanzia asubuhi hadi usiku, hivyo kusababisha washindwe kuzingatia masomo yao shuleni.

Aidha, alisema wapo watoto wengine wamekuwa wakishinda kwenye sehemu zinazoendesha michezo ya kamari kinyume na sheria, ambapo aliagiza pia watu hao wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Hapi alionya kama wazazi wasipokuwa makini kutoa taarifa juu ya vibanda ambavyo watoto wanaingia kushiriki mchezo huo, watatengeneza kizazi cha wajinga, kitu ambacho hawatakiwi kuruhusu kitokee.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *