Jiji la Dar es Salaam limepitisha bajeti ya zaidi ya Sh bilioni 20 ambayo imejikita katika kumalizia miradi inayoendelea na kutekeleza miradi mipya.

Bajeti hiyo ni ongezeko maradufu la bajeti ya mwaka uliopita ambayo ilikuwa ni Sh bilioni 7.7 Akisoma bajeti hiyo kwa maelekezo ya Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Mussa Kafana, Mbunge wa Ubungo, Saaed Kubenea amesema kwamba bajeti ya maendeleo imefikia asilimia 62 ya bajeti nzima.

Amsema vipaumbele vya bajeti ni pamoja na kuboresha mapato na kudhibiti mianya ya upotevu kwa kutumia mifumo ya kielektroniki, uwekezaji vitega uchumi katika viwanja vya Jiji, ujenzi na ukarabati wa majengo, barabara na vituo vya mabasi yaendayo mikoani Mbezi Luis na Boko.

Akichambua bajeti hiyo Kubenea amesema kwamba kati ya Sh 20,278,441,110.00, Sh 3,2133,512,000.00 ni ruzuku kutoka serikali kuu na Sh 17,144,929,110.00 ni makusanyo ya ndani.

Aidha kati ya mapato hayo kiasi cha Sh 6,674,688,000 ni mapato ya kugawana na Halmashauri za manispaa na hivyo jumla ya Sh 10,470,241,110.00 ni mapato ya ndani yatakayotumika kugharamia matumizi ya kawaida, mishahara ya watumishi pamoja na miradi ya maendeleo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *