Serikali imesema kuwa itatoa adhabu kali ya kifungo cha miaka 30 jela kwa wazazi wote wawili wa mtoto wa kike atakayekatishwa masomo na kulazimishwa kuolewa ama akipata ujauzito.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wilayani Hanang mkoani Manyara katika ziara yake ya kikazi ya siku sita mkoani humo.

Amesema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kumlinda mtoto wa kike katika kuhakikisha kuwa anapata haki yake ya msingi ya kusoma kufikia elimu ya chuo kikuu kwa kujenga mabweni na kuwachukulia hatua kali za kisheria watu watakaowapa mimba na kuwaozesha katika umri mdogo na kukatisha masomo yao.

Amesisitiza kuwa kupitia sera ya kuboresha elimu nchini serikali imeondoa michango ya fedha za kulipia bili za maji, umeme, gharama za mlinzi na mitihani ili kumpunguzia gharama mzazi na mlezi na kuwaacha wazazi kushughulikia maeneo mengine muhimu kwa mtoto wao.

Pia amesema tayari kwa mwaka huu wa fedha, walimu 4,396 wa masomo ya sayansi wameajiriwa ambapo alisisitiza kuwa wazazi na walezi wanalo jukumu kubwa la kusimamia maendeleo ya shule ya watoto wao kwa lengo la kupandisha ufaulu wa elimu kwa wilaya,mkoa na taifa.

Akizungumza na watumishi wa umma katika halmashauri ya wilaya hiyo, aliwataka watumishi hao kujivunia serikali yao kwa kuienzi katika kufanya kazi kwa nidhamu katika kuwatumikia wananchi bila kujali uwezo wao, kabila wala rangi zao kwa kuwa wamepewa dhamana ya kusikiliza kero zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *