Kesi ya wanafunzi wanne wa Chuo Kikuu cha Kampala cha jijini Dar es Salaam imesikilizwa Mahakama ya Wilaya ya Ilala hapo jana.

Wanafunzi hao wanakabiliwa na shitaka la kuchapisha picha zinazoonyesha Rais Dk. John Magufuli amevaa hijabu kama mwanamke wa Kislamu na kuzisambaza kwenye mtandao wa WhatsApp.

Pia wanafunzi hao wanakabiliwa na shtaka la kusambaza taarifa za uongo kwenye mitandao ya  amii (WhatsApp) kwa lengo la kumuudhi Rais.

Washitakiwa hao ni Amenitha Kongo (19), Maria Tweve (20), Agnes Gabriel (21) na Anne Mwansasu(21).

Akisoma mashitaka hayo, Wakili wa Serikali, Florida Wenceslaus amedai washitakiwa walitenda kosa hilo Juni 9 mwaka jana  Dar es Salaam.

Wakili huyo amedai washitakiwa kwa pamoja walitengeneza picha hizo kwa kutumia kompyuta na baadaye kuisambaza kwenye WhatsApp kwa lengo la kumuudhi Rais.

Washitakiwa hao wamekana shitaka hilo na kurudishwa rumande kutokana na kutotimiza masharti ya dhamana.  Kesi itatajwa tena Machi 13 mwaka huu.

Source: Mtanzania

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *