Video Queen maarufu Bongo, Agnes Gerald ‘Masogange’ ameendelea kusota rumande huku jalada la kesi yake likiwa mikononi mwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Masogange mwenye umri wa miaka 25 alikamatwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa tuhuma za kujihusisha na kuuza, kusafirisha na kutumia dawa za kulevya.
Wiki iliyopita alitarajiwa kupandishwa kizimbani lakini ilishindikana kutokana na majibu ya Mkemia Mkuu wa Serikali ya vipimo vya kuonesha kama anatumia au hatumii dawa hizo kutokamilika.
Wakili wa Masogange, Nick Kitege amesema anaendelea kulifanyia kazi suala hilo na pindi litakapokamilika muda wowote anaweza kupelekwa mahakamani.
Kitege amesema kuwa “Kuhusu ucheleweshwaji wa kesi hiyo ni kutokana na taratibu za kisheria, hivyo Polisi waachwe wafanye kazi yao na sisi tunaangalia hatua zinazoendelea, unajua hivi ni vyombo vya sheria na wanafanya kazi yao, wanahitaji muda kuchunguza na kutoa hoja zilizojitosheleza, bado wanahangaika kushughulikia suala hilo naamini leo tutapata jibu kamili juu hatua inayofuata,”.
Masogange ni miongoni mwa watu maarufu waliokamatwa kwa kujihusisha na masuala ya dawa za kulevya nchini kwenye vita iliyoanzishwa na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.