Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Freeman Mbowe jana amejisalimisha katika Kituo Kikuu cha Polisi Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na sakata linaloendelea la vita dhidi ya dawa za kulevya.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Simon Siro ndiye aliyetoa wito wa kumtaka, Mbowe kuwasili kituoni hapo, ikiwa imepita takribani wiki mbili tangu jina la kiongozi huyo wa Kambi ya Upinzani Bungeni kuwa ndani ya orodha ya watu sitini na tano ambao Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewataka waende kituoni hapo kwa ajili ya mahojiano.
Taarifa za kujisalimisha kwa Mbowe zimethibitishwa na Msemaji wa Chadema Bw. Tumaini Makene ambaye hakutoa taarifa za undani wa nini kinaendelea hivi sasa ingawa kuna taarifa kwamba baadhi ya viongozi wa juu wa Chadema wanakutana katika kikao cha dharura kujadili suala hilo.
Hadi majira ya saa moja na nusu usiku hapakuwa na taarifa yoyote rasmi kutoka kituoni hapo, ingawa taarifa isiyo rasmi inadai kuwa Mbowe aliondolewa kituoni hapo akiwa katika gari tofauti na haikufahamika ni wapi amepelekwa.