Meli mbili za MV Ruvuma na MV Njombe zinatarajiwa kukamilika na kukabidhiwa katika bandari ya Itungi wilayani Kyela mkoani Mbeya mwezi ujao.
Ujenzi huo umekamilika kwa zaidi ya asilimia 98 na kwamba meli hizo zinatarajiwa kufanyiwa majaribio Ziwa Nyasa mwishoni mwa mwezi huu na kukabidhiwa rasmi serikalini mwezi ujao.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro Marine Transport Ltd ya jijini Mwanza inayounda meli hizo, Saleh Songoro.
Sonoro amesema kukamilika kwa meli hizo mbili za mizigo za kisasa zenye uwezo wa kubeba tani 1,000 za mizigo kila moja na kugharimu Sh bilioni 11, kutaiwezesha kampuni hiyo kuanza kuunda meli nyingine ya tatu itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 200 za mizigo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda na Naibu Katibu Mkuu Fedha na Mipango pamoja na kupongeza kazi kubwa iliyofanywa na mkandarasi mzawa, Songoro Marine Transport Ltd, kuunda meli hizo, wamesema kuwa kukamilika kwa meli hizo kutachochea biashara na mapato ya serikali kupitia shughuli za usafiri na usafirishaji katika Ziwa Nyasa.
Profesa Mkenda amesisitiza kuwa serikali itaangalia uwezekano wa kumtumia mkandarasi huyo kuunda meli nyingi zaidi za ndani na nje ya nchi ili kukamata soko hilo la utengenezaji wa meli kitaifa na kimataifa hatua itakayoliletea Taifa sifa, kukuza uwekezaji na ajira.