Ubunge wa Ester Bulaya ambaye ni mbunge wa Bunda upo mashakani baada ya Wapiga kura wanne wa Jimbo hilo kufungua shauri kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliopita kwenye jimbo la Bunda.
Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Francis Kabwe amesema kuwa rufaa ya wapiga kura hao, Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Acetic Malagila iliyosajiliwa kwa namba 199 ya mwaka 2016, itasikilizwa mfululizo kuanzia Februari 20.
Pia amesema rufaa hiyo itasikilizwa jijini Mwanza na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, Salim Mbarouk, Augustine Mwarija na Shabani Lila.
Wapigakura hao wanaowakilishwa na Wakili Constantine Mutalemwa, wanaiomba Mahakama kutengua ushindi wa Bulaya dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Stephen Wasira kwa madai kuwa uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka 2015 haukuwa huru na wa haki.
Masato na wenzake wanadai kuwa mchakato wa kampeni, upigaji kura na utangazaji wa matokeo uligubikwa na ukiukwaji wa sheria na utaratibu wa uchaguzi, vikiwamo vitendo vya rushwa, msimamizi wa uchaguzi kumnyima haki Wasira kwa kukataa ombi lake la kura kuhesabiwa upya.
Novemba 17, mwaka jana, Jaji Noel Chocha wa Mahakama Kuu alimtangaza Bulaya kuwa mshindi halali wa uchaguzi huo baada ya kutupilia mbali maombi ya wapigakura hao.