Zaidi ya watanzania 132 wanaoishi nchini Msumbiji wamefukuzwa nchini humo huku wengine wasiojulikana wakidaiwa kukamatwa kufuatia operesheni ilioanzishwa na serikali ya taifa hilo.
Kulingana na serikali ya Msumbiji operesheni hiyo inalenga kuwatimua raia wa kigeni wanaoishi nchini humo kinyume cha sheria.
Taarifa ya wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika mashariki nchini Tanzania imesema kuwa raia waliofukuzwa ama hata kukamatwa ni wale wanaoishi mji wa Monte Puez kwa kuwa una raia wengi wa kigeni ikilinganishwa na miji mingine.
Kulingana na taarifa hiyo tayari ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji unaendelea kufanya mawasiliano ya kidiplomasia na serikali ya Msumbiji ili kuwahakikishia usalama raia wa Tanzania na mali yao nchini humo.
Inakadiriwa kuwa, Watanzania wapatao elfu tatu (3,000) wanaishi na kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii katika mji huo wa Monte Puez.