Mshauri mkuu wa ikulu ya White House kuhusu usalama wa taifa Michael Flynn amejiuzulu kuhusiana na uhusiano wake na maafisa wa Urusi.
Flynn anadaiwa kujadili vikwazo vya Marekani dhidi ya Urusi akiwa na balozi wa Urusi kabla ya Rais Donald Trump kuingia madarakani.
Anadaiwa kuwapotosha maafisa wa utawala huo mpya kuhusu mazungumzo yake na balozi huyo.
Awali, vyombo vya habari Marekani viliripoti kwamba Wizara ya Haki ilitahadharisha ikulu ya White House mapema kuhusu mawasiliano ya Flynn na maafisa wa Urusi mwishoni mwa mwezi uliopita.
Maafisa wakuu wa chama cha Democratic walikuwa wametoa wito kwa Bw Flynn kuachishwa kazi.
Mashirika ya habari ya Associated Press na Washington Post yanasema wizara ya haki Marekani ilitahadharisha kuhusu kile ilichosema ni mambo aliyoyasema Bw Flynn kuhusu mazungumzo yake na balozi wa Urusi.
Ni kinyume cha sheria kwa raia wa kawaida kujihusisha na shughuli za kidiplomasia Marekani.
Mazungumzo kati ya Flynn na balozi wa Urusi yanadaiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka jana, kabla ya Bw Flynn kuteuliwa kuhudumu katika uatawala wa Bw Trump.