Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amesema kuwa ni kinyume na sheria wabunge kukamatwa wanapokuwa katika vikao vya Bunge.

 

Ndugai amesema kama kuna kiongozi yeyote wa serikali anamuhitaji mbunge, anapaswa kutoa taarifa kwake kwanza badala ya kwenda kumkamata.

 

Pia Ndugai amewatoa hofu wabunge kuhusu hadhi ya Bunge na kusema kuwa hadhi ya chombo hicho haijashuka, na kwamba Muhimili huo wa Bunge hauna mgogoro wowote na serikali wala mahakama.

 

 

Hatua hiyo inafuatia malalamiko ya wabunge wa upinzani yaliyotolewa hivi karibuni juu ya utaratibu unaotumiwa na Jeshi la Polisi kukamata wabunge wanapokuwa kwenye vikao vya Bunge, wakitolea mfano wabunge Tundu Lissu na Godbless Lema.

 

Malalamiko hayo yalifikia hatua ya mbunge Zitto Kabwe kutoa hoja akitaka kiti cha Spika kitoe maamuzi ya kulinda hadhi ya Bunge kutokana na kukamatwa kwa Tundu Lissu, hoja ambayo Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson aliipangua, jambo lililopelekea wabunge wote wa upinzani wasusie kikao cha Bunge cha jioni ya Februari 8, 2017.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *