Mahakama Kuu nchini Kenya imebatilisha uamuzi wa serikali ya nchi hiyo kufunga kambi ya wakimbizi ya Daadab.
Mahakama hiyo imesema kuwa waziri wa usalama wa ndani, Meja Jenerali mstaafu Joseph Nkaissery alikiuka katiba wakati wa kutoa agizo la kufungwa kwa kambi hiyo.
Jaji JM Mativo amesema agizo la serikali lilibagua na lilikuwa sawa na kuadhibu watu kwa pamoja.
Jaji huyo alikuwa anatoa uamuzi katika kesi iliyowasilishwa na mashirika mawili ya kutetea haki za kibinadamu ambayo ni Shirika la Taifa la Haki za Kibinadamu na Kituo Cha Sheria, yakisaidiwa na shirika la kimataifa la Amnesty International.
Serikali awali ilitangaza kwamba ingefunga kambi hiyo, ambayo ndiyo kubwa zaidi duniani ili kulinda Kenya dhidi ya mashambulio ya kigaidi.
Kambi hiyo inatoa hifadhi kwa wakimbizi 260,000, ambapo wengi wao kutoka nchi jirani ya Somalia.