Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo ‘Mzee wa Upako’ amesema kuwa yeye ni mmoja kati ya watu ambao wamewahi kutuhumiwa kuhusika na biashara ya dawa za kulevya.
Mzee wa Upako amesema hayo baada ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwataja watu mashuhuri wanaojihusisha na uuzaji wa madawa ya kulevya ambao ni Freeman Mbowe, Mchungaji Josephat Gwajima, Yusuf Manji na Idd Azzan.
Mchungaji huyo amesema kuwa kuwa yeye ni mhanga wa suala hilo jambo ambalo lilimpa wakati mgumu sana katika maisha na kumfanya kunyanyapaliwa na jamii pamoja na watu wake wa karibu wakiwemo wachungaji wenzake.
Lusekelo amesema kuwa mwaka 1997 alituhumiwa kuuza dawa za kulevya lakini anakiri wazi kuwa polisi wa kipindi kile walikuwa ni wastaraabu kwani waliamuandikia samansi na kumuomba kufika kituo cha polisi kutoa maelezo.
Mzee wa Upako ameshauri vita ya dawa za kulevya kwa watu wanaotuhumiwa ni bora viongozi wangetumia njia za kipolisi kuwataka kufika polisi kwani kutumia njia ya magazeti inaweza kushusha heshima ya baadhi ya watu ambayo wameijenga kwa miaka mingi.
Amesema yeye binafsi anachukia sana dawa za kulevya kutokana na madhara yake kwa jamii, hivyo hawezi kuthubutu kujihusisha nazo wala hawezi kuunga mkono watu wanaofanya shughuli hizo kwa kuwa dawa za kulevya zinaua kizazi cha maendeleo na taifa kwa ujumla.