Wabunge  wa vyama vya upinzani jana wametoka nje ya Bunge  wakipinga wenzao kufukuzwa bungeni pamoja na kitendo cha kukamatwa kwa Mbunge Singida Mashariki Tundu Lissu.

Wabunge waliokuwa wameamuliwa kutoka nje ya ukumbi wa Bunge na Naibu Spika Dkt Tulia Ackson ni pamoja na mbunge wa Kawe Halima Mdee, Mbunge wa Bunda Mjini Ester Bulaya na Mbunge wa Serengeti Marwa Ryoba.

Wabunge hao watatu wamedaiwa kupinga uamuzi wa Naibu Spika kuhusu muongozo ulioombwa na mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe, kuhusu utaratibu uliotumika kumkamata mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Mara baada ya Naibu Spika kutoa maamuzi ya kuwaondoa wabunge hao watatu bungeni, ndipo wabunge wengine wa upinzani pia wakaamua kutoka kama ishara ya kupinga maamuzi hayo, pia ikiwa ni ishara ya kupinga utaratibu wa kukamatwa kwa mbunge Tundu Lissu.

Nje ya ukumbi wa Bunge, Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe, amesema wamefikia hatua hiyo kuonesha kuwa uataratibu unaotumiwa kukamata wabunge wakiwa bungeni siyo sahihi, na kwamba kesho wataendelea na vikao vya bunge lakini mapambano yataendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *